Skip to main content

Newsletter block in header

prev
next

You are here

Taarifa ya operesheni za MSF nchini Kenya

MSF linafanyia kazi kuanza kuzoea programu za kitabibu nchini Kenya ili kukabiliana na mlipuko wa COVID-19

Hata ile mifumo ya afya katika nchi zilizoendelea duniani imezidiwa uwezo kutokana na mlipuko huu, kwa hivyo tuna wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa athari zake nchini Kenya, na ukubwa wa msaada ambao utahitajika

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), linafanyia kazi kuanza kuzoea programu za kitabibu nchini Kenya ili kukabiliana na mlipuko wa COVID-19.

Timu zinafanya kazi kuboresha vituo vya kuzuia na udhibiti, kutengeneza vituo vya dharura vya matibabu, vituo va upimaji, vyumba vya kutenga wagonjwa na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya, kutoa ushauri katika vituo vinavyotumika kuwatenga wagonjwa na kusambaza ujumbe wa uhamasishaji.

Nchini Kenya na maeneo mengine duniani, MSF inaguswa hasa na athari za mlipuko huu zitakazowapata watu walio kwenye mazingira magumu. Wale ambao wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi au walioko kwenye kambi za wakimbizi ambao wako hatarini zaidi – maeneo haya mara nyingi huwa na idadi kubwa ya watu na watu hukosa baadhi ya huduma za msingi za usafi ikiwemo maji safi na salama.

“Tunawasiwasi sana kuhusu mlipuko kufika kwenye maeneo yenye watu wengi kama vile Mathare na Kibera jijini Nairobi na kwenye kambi za wakimbizi kama vile Dadaab,”anasema Lili-Marie Wangari, mratibu wa masuala ya dharura wa MSF. “Hivi sasa, watu wanahitaji haraka upatikanaji wa maji ili waweze kuosha mikono yao, pamoja na taarifa kuhusu namna wanavyoweza kujilinda na familia zao. Ikiwa virusi vitaenea katika maeneo haya, tutahitaji hatua ya haraka ili kuudhibiti.”

Timu ya MSF ya watu saba inasaidia kituo cha afya cha Kibera Kusini kwenye eneo la Kibera jijini Nairobi, ambako wanaongeza nguvu katika mkakati wa kuzuia, wametengeneza vituo vya upimaji na vituo vya huduma za dharura pamoja na maeneo ya watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi.

Katika siku za usoni timu ya MSF ina mpango wa kuweka vituo vya maji zaidi ya 60 kwenye maeneo ya Mathare na Kibera ili kusaidia watu kuosha mikono yao. Pia wataongeza watu zaidi ambao wataenda kwenye jamii kutoa uelewa zaidi kuhusu ugonjwa huu.

Pamoja na kuwa sehemu ya timu ya kikosi kazi cha taifa katika kukabiliana na Covid-19 kikosi kazi ambacho kinakutana mara mbili kwa wiki kuratibu majadiliano kuhusu namna bora nchi inaweza kujiandaa kukabiliana na mlipuko, MSF inafanya kazi na vitengo vya afya katika kaunti ambazo ina miradi – Embu, Kiambu, Mombasa, Garissa, Nairobi na Homa Bay. Kukiwa na mpango mkakati kama huu wa kina kujiandaa katika kukabiliana na COVID-19, uratibu baina ya timu zinazoshughulikia janga hili ni muhimu sana.

“Miongoni mwa vipaumbele vyetu ni pamoja na kuhakikisha programu zetu zinaendelea kufanya kazi kwaajili ya wagonjwa na jamii ambazo ziko kwenye mazingira magumu, akina mama wataendelea kujifungua na watu wataendelea kuhitaji huduma za dharura wakati wote wa mlipuko,” anasema Dr Mohammed Musoke, mratibu wa matibabu wa MSF nchini Kenya. “Ili kuwaweka watu salama, tunaweka mpango wa namna tunaweza wahudumia wagonjwa kama vile wale wa HIV na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza hadi kwa zaidi ya miezi mitatu’ kusambaza dawa wanazohitaji, kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi wakiwa katika vituo.

Kuwalinda wafanyakazi wa afya na wagonjwa ni suala ambalo linasalia kuwa la msingi kwa MSF na inahakikisha inaweka mikakati ya kutosha ya kuzuia maambukizi na udhibiti, kutenga maeneo maalumu ya vipimo na vituo vya dharura maeneo ya kutenga watu na kutoa elimu ya afya. Katika baadhi ya vituo ambako inafanya kazi, MSF imetenga vyumba maalumu vya kuwatenga wagonjwa, na inatengeneza uwezo wa kuwahudumia wagonjwa ambao watagundulika kuwa na maambukizi ya COVID-19 katika kambi ya Dagahaley.

“Hata ile mifumo ya afya katika nchi zilizoendelea duniani imezidiwa uwezo kutokana na mlipuko huu, kwa hivyo tuna wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa athari zake nchini Kenya, na ukubwa wa msaada ambao utahitajika” anasema Anne Cugier, Mkurugenzi wa MSF nchini Kenya.”Uwezo wetu wa kukabiliana na mlipuko huu pia utaathirika kutokana na changamoto tunazokabiliwa nazo kama za wafanyakazi na upatikanaji wa vifaa, hasa vifaa kinga binafsi ambavyo vinahitajika ili kuwaweka wafanyakazi wa afya na wagonjwa salama, kwa hivyo timu yetu inajaribu kufanya kile inachoweza kuwasaidia watu ambao wana uhitaji zaidi.”

 Programu za matibabu za MSF nchini Kenya na kukabiliana na COVID-19 Kenya

 Kituo cha afya Kibera: 

MSF inasaidia kituo cha afya cha Kibera Kusini, kwenye eneo la Kibera, eneo kubwa zaidi la makazi lenye msongamano wa watu jijini Nairobi, ni kituo cha afya kilichojengwa na awali kilikuwa kinatumiwa na shirika. Timu ya watu saba inasaidia kuweka mkakati wa kuzuia na udhibiti, vituo vya huduma za dharura, upimaji na kuwahamisha wagonjwa wanaohisiwa katika hospitali jirani. Hivi karibuni wataweka vituo vya maji katika jamii inayozunguka, na kuongeza idadi ya watu watakaosaidia kupeleka ujumbe wa uhamasishaji.

Kutibu magonjwa yasiyoambukiza Embu: 

Tangu mwaka 2017, MSF imekuwa ikifanya kazi Embu kuhuisha utoaji matibabu wa magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali wa uma. Zaidi ya wagonjwa 4,000 waliokuwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza walisajiliwa kupewa huduma katika vituo vya afya 11. katika kujiandaa na Covid-19, MSF imesaidia vituo hivi 11 kuwa na uwezo wa kuzuia na kudhibiti na kutoa elimu kwa wagonjwa na wafanyakazi. Shirika pia linasaidia hospitali ya ngazi ya tano ya Embu kwa kuwa na huduma za dharura na kupima wagonjwa.

Kutibu wagonjwa wa HIV Homa Bay: 

Katika hospitali ya rufaa ya Homa Bay, MSF inatoa msaada katika wodi ya watu wazima ikiwa na vitanda 90. Msf imeendelea kufanya kazi katika kuboresha huduma za HIV na kupunguza maambukzi na vifo mjini Homa Bay. Wakati huu kukiwa na mlipuko wa COVID-19, Msf imetoa dawa za ARVs za miezi mitatu kwa wagonjwa ili kuwalinda dhidi ya kupata maambukizi hospitalini. Timu yetu imetenga eneo la huduma za dharura, vipimo na vyumba vya kutenga wagonjwa katika hospitali ili kusaidia kujiandaa kwa mlipuko.

Pia, MSF imeisaidia timu ya kaunti kutengeneza kituo kwaajili ya kuwahudumia watu waliothibitishwa kuwa na Covid-19 kwenye eneo la Malela na kutoa msaada wa usafiri na mafunzo kwa wafanyakazi wote hasa kuhusu udhibiti na kuzuia (IPC).

Kuhudumia watu ambao walikuwa wanatumia dawa, Kiambu: 

MSF inatoa huduma ya kituo cha pamoja kwa watumiaji dawa, ikijumuisha utoaji tiba mbadala, matibabu ya HIV, TB, Homa ya ini aina C na magonjwa yasiyoambukiza, kusafisha vidonda, afya ya akili na ushauri nasaha, elimu ya ngono na uzazi katika kliniki ya Kiambu. Kliniki ya tiba mbadala ilifunguliwa mwezi September mwaka 2019 na leo hii, zaidi ya watu 150 ambao wanatumia dawa wameingizwa kwenye mradi. MSF imetengeneza mfumo wa huduma za dharura na vyumba vya kutenga wagonjwa, pia inafanya kazi katika hospitali jirani ya Karuri ili kuongeza nguvu katika juhudi za udhibiti na kuzuia.

Kuwahudumia wahanga wa vitendo vya ukatili, Mathare:

MSF ina chumba cha ushauri kwenye eneo la Mathare, jijini Nairobi, ikitibu wahanga wa vitendo vya ukatili mijini kwenye eneo la Eastlands. Kliniki hii inafanya kazi saa 24, kituo cha huduma za simu bure na programu za magari ya wagonjwa ambayo yanatoa huduma kwa wagojwa na kuwapeleka katika vituo vikubwa vya matibabu pale inapohitajika. Gari la wagonjwa limegeuzwa na kuanza kutumika kwaajili ya wagonjwa wa COVID-19.

MSF pia inatoa huduma maalumu kwaajili ya wahanga wa vitendo vya ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia kwenye eneo la Eastlands na pia kwa kusaidia vituo vya wizara ya afya. Timu zetu zinatoa msaada wa kisaikolojia kwa njia ya simu na kuendelea kuwahudumia watu katika kipindi chote cha mlipuko. Pia wameendelea kufanya kampeni ili kuhakikisha kuwa watu wanafahamu kuwa bado wapo.

Huduma za matibabu kwa wakimbizi: 

Katika kambi ya Dagahaley, Dadaab, kambi kubwa zaidi ya wakimbizi nchini Kenya, MSF inahudumia hospitali yenye vitanda 100 na vituo viwili vya afya. MSF inatoa huduma za afya kwa wakimbizi, wengi wakiwa wameishi katika kambi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, lakini pia kwa jamii inayozunguka. Hospitali ya hapa inatoa huduma zote za awali na zile za kiwango cha juu.

Timu yetu inaweka mikakati ya kuhakikisha kunakuwepo uwezo wa kutosha wa udhibiti wa maambukizi, kuongeza kasi ya upimaji katika vituo vya huduma za dharura, eneo la kutenga watu na kutoa elimu ya afya. Kwa sasa kuna eneo la kutenga watu lenye vitanda 10 kwa washukiwa wa ugonjwa wa Covid-19 na kunauwezekano wa kuongeza vitanda hadi kufikia 40 ikiwa itahitajika. Kitengo hiki kitageuzwa na kuwa kituo cha matibabu pale itakapotokea mlipuko ni mkubwa kwenye jamii au pale ambapo huduma nyingine kwaajili ya wagonjwa hazitakuwepo. Mafunzo kwa wafanyakazi wa afya ili kutengeneza mnyororo wa watu watakaokuwa mstari wa mbele yanaendelea.

Huduma msingi kwa ajili ya uzazi katika eneo la Likoni: 

Katika kaunti ndogo ya Likoni, mjini Mombasa, MSF inasaidia kitengo cha wizara ya afya kutoa huduma za dharura za uzazi na watoto katika kituo kipya kabisa kilichokarabatiwa cha Mrima. Timu yetu huko inasaidia angalau kwa wastani akina mama 7,000 kujifungua kila mwaka, wakifanya upasuaji wa kuokoa maisha na kutoa huduma za kabla na baada ya kujifungua, pamoja na huduma za wagonjwa wa saratani ya uzazi, HIV na magonjwa mengine ya zinaa. Kujiandaa na COVID-19 timu yetu imetengeneza vyumba maalumu vya kutenga wagonjwa, vyumba ambavyo vitaruhusu akina mama ambao wana COVID-19 kujifungua salama.

Keywords

Change country