Kupungua kwa matumaini ya suluhu ya kudumu wakati huu kukiendelea kushuhudiwa hali tete ya usalama nchini Somalia na hali mbaya ugavi wa malazi kumesababisha kufurika kwa wakimbizi kwenye kambi ya Dadaab huku wengi wakiwa tegemezi. Huku kukiwa na hali mbaya ya uwezo wa kutoa huduma na njia za kujikimu, misaada ya kibinadamu bado imesalia kuwa ya muhimu sana kwa maisha ya wakimbizi. Lakini kuishi kwa kutegemea msaada duni ina maana kuwa wengi wamekuwa wakiishi kwa dharura kwa karibu miongo mitatu sasa. Mahitaji yao yanazidi hata kiwango cha misaada ya kibinadamu inayotolewa wakati huu hata wfadhili wakisuasua kuchangia.
Janai Issack alikuwa na miaka 10 wakati alihamia katika kambi na familia yake mwaka 1991m akikimbia machafuko Somalia. “Mambo mengi yamebadilika kwa miaka kadhaa: Nimeolewa, nimezalia hapa, na wote tunaishi pamoja katika eneo hili,” anasema. “Maisha yalikuwa mazuri wakatyi tulipowasili kwa mara ya kwanza kambini. Usalama tulioukuta hapa ulikuwa ahueni ukilinganisha na kile kilichokuwa kikitokea Somalia, na usaidizi kutoka mashirika ya misaada ulikuwa mzuri.”
Janai analalamika kuwa kwa miaka kadhaa, idadi na ubora wa huduma zilizokuwa zikitolewa kwa wakimbizi zimepungua. “Mgawanyo wa chakula pia umepunguzwa. Kwa sasa tunapewa chakula kidogo ambacho hakiwezi hata kutukimu kwa wiki kadhaa. Madarasa ambayo watoto wetu walikuwa wakienda kusoma sasa yamefurika, tofauti na wakati ule nilipokuwa nikienda shule,” anasema, “Nafikiri UNHCR imechoka. Sijui ni kwanini wanaendelea kutuuliza ikiwa tunataka kurejea Somalia, huku bado majibu yetu yakiwa ni yale yale kama ya awali: Hapana. Mgawanyo pia umbadilika kuanzia mwaka uliopita, ni kama vile hakuna mtu anayeenda popote.”
Wakimbizi wengi kwenye kambi ya Dagahaley – moja ya kambi tatu ambazo zinaunda Dadaab, ikiwa na idadi ya watu elfu 75 – nao wana ushuhuda sawa na wa Janai. Wanalalamikia kupungua kwa misaada, kama vile mgawanyo wa chakula. Shirika la umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP, mwezi Septemba lililazimika kupunguza zaidi mgwanyo wa jumla wa chakula katika kambi za wakimbizi kwa zaidi ya asilimia 70 ya mgawanyo wa kawaida, kutokana na uhaba mkubwa wa fedha. Hali hii huenda ikasababisha athari mbaya za kiafya kwa wakimbizi, kama ambavyo MSF imeshuhudia katika miaka ya nyuma.
“Kwa watu wengi, maisha katika kambi ndio kitu wanakijua,” anasema Dana Krause, muwakilishi wa shirika la Madaktari Wasio na Mipaka nchini Kenya. “Lakini kuishi katika kambi kwa miongo mitatu huku ukipokea chakula kidogo, kukosa huduma muhimu za afya na hakuna ajira, au hata kiinua mgongo cha kufanya kazi, hakuna zaidi ya kusema ni mashambulizi dhudu ya utu wa binadamu.”
Kwa Abdia mwenye umri wa miama 65, ambaye alikimbia Somalia mwaka 1991, maisha katika kambi yamezidi kuwa mabaya. “Kama nikilinganisha maisha yangu ya sasa na vile yalikuwa miongo miwili iliyopita, hali ilikuwa bora zaidi wakati ule. Mgawanyo wa chakula ni mdogo na ukiwa mtu mwenye umri mkubwa ambaye huna mtu wa kukuhudumia, utaona maisha magumu sana,” anasema, “Utoaji wetu wa huduma una kiwango, na huduma zimepungua kwa kiwango kikubwa.”
Kwa wakimbizi ambao hawajasajiliwa, mapambano ya kupata huduma za msingi katika makambi yanakuwa magumu zaidi, kwa mujibu wa UNHCR, kuna zaidi ya waomba hifadhi elfu 15 ambao hawajasajiliwa, na ni karibu nusu yao tu ndio wanapokea msaada wa chakula kwa kuzingatia tathmini na hali waliyonayo. Licha ya kuwa wakimbizi ambao hawajasajiliwa wanaweza kupata huduma za MSF kwenye kambi ya Dagahaley, kwa mahitaji mengine zaidi, ikiwemo malazi na nguo wanaachiwa kutafuta wenyewe.
Kuzorota kwa afya ya akili na mapambano ya kupata huduma bora za afya
Kwa wengine kama Abdo Mohamed Geda mwenye umri wa miaka 42 ambaye alikuja kwenye kambi ya Dadaab mwaka 2011 amelazimika kufanya kazi za kawaida ili kufidia ombwe la mgawanyo wa chakula wanachopokea kwa sasa. Abdo anatafuta kuni kwa kutumia punda ili kuilisha familia yake ya watoto nane. “Watoto wanahitaji maziwa, chakula na mavazi,” anasema. “Kila asubuhi ninatoka kwenda kutafuta chakula kwaajili ya familia yangu. Lakini pale kunapokuwa hakuna kitu, napata msongo wa mawazo. Siwezi kulala.” Abdo kwa sasa anaendelea kupata matibabu ya msongo wa mawazo katika hospitali ya MSF kwenye kambi ya Dagahaley.
Kutolewa katika mahema ya muda kumedidimiza matumaini ya watu kuwa na afya njema na maisha mazuri. Na hili limedhihirika wazi kutokana na matatizo makubwa ya akili yanayowakumba. Kwa wastani, kambi ya Dagahaley peke yake, MSF inatoa msaada wa mashauriano kwa watu elfu 5,500 wenye matatizo ya afya ya akili kila mwaka. Wakati wa shinikizo kubwa idadi hii mara nyingi huongezeka kama ilivyokuwa mwaka 2016, wakati vitisho vya kuzifunga kambi hizo vilipozidi.
Mwezi Octoba mwaka huu, MSF iliwatibu wagonjwa wawili ambao walijaribu kutoa uhai wao kwenye kambi ya Dagahaley. Mmoja katik yao ni mkimbizi ambaye hakuwa amesajiliwa kutokea Somalia, alijaribu kujinyonga kabla ya kuokolewa. Amekuwa akiishi kwa kuombaomba tangu kadi yake ilipozuiwa mwaka 2018. Lakini kadiri mgawanyo wa chakula ulivyoendelea kupunguzwa katika miezi ya hivi karibuni, majirani wanalazimika kuishi kwa chakula kidogo ambacho wanapokea. Wagonjwa wote kwa sasa wanaendelea na matibabu na wanapokea msaada wa kisaikolojia.
Huduma mahsusi za afya bado hazitolewi kwa wakimbizi wengi. Licha ya kuwa MSF inatoa huduma za afya za awali na zile za juu kwenye kambi ya Dadaab, huduma za kiwango cha juu au zile mahsusi zinahitaji wagonjwa kuhamishwa nje ya kambi. Lakini kwakuwa uhuru wao umewekewa mipaka, ni wale tu wanaohitaji huduma za dharura, huduma za kuokoa maisha ndio wanaoruhusiwa na wanasaidiwa kupata matibabu katika hospitali ya Garissa au Nairobi. Kwa hivyo idadi ya watu wanaohitaji huduma mahsusi za afya imeendelea kuongezeka kila mwaka, na kuweka msururu mrefu wa wagonjwa wanaosubiri kutibiwa. Kwenye kambi ya Dagahaley peke yake, zaidi ya watu elfu 1,100 wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa kawaida na wengine wanasubiri kupatiwa huduma mahsusi za afya.
Uhitaji wa haraka kupata suluhu
“Ikiwa uwajibikaji kuboresha hali za wakimbizi kwa kuzingatia athari za kidunia zinazowakabili wakimbizi unataka kufikiwa, basi ni muda kwa serikali ya Kenya na Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua stahiki kutafuta njia mbadala kwa wakimbizi nje ya kambi,” anasema Krause. “Sera ambazo zinasaidia uhuru wa wakimbizi kutembea na upatikanaji wa huduma za msingi, na kuchagizwa na uwekezaji wa wafadhili katika kuwajengea uwezo, kutaruhusu wakimbizi kuishi maisha yenye utu, na wakati huohuo kunufaisha halaiki.”
Mpaka sasa, suluhu pekee iliyopendekezwa katika mzozo huu wa wakimbizi ni kufungwa kwa kambi. Lakini asilimia kubwa ya wakimbizi wako tayari kurudi nyumbani. Miongoni mwa wale waliorudi, wengi wamerejea kwenye kambi ya Dadaab wakieleza kuwepo kwa hali tete ya usalama na ukosefu wa huduma muhimu kwenye nchi yao. Na mpango wa kuwahamishia katika mataifa mengine unaonekana kufa kwa sasa.
“Kwa kufanya kuwa vigumu kuishi kwenye kambi, tunahisi ni kana kwamba tunakunjwa mikono ili turudi”, anasema Geda. “Ikiwa hali itasalia kama ilivyo, tutalazimika kurejea. Tuna matumaini kuwa siku moja nchi yetu itakuwa salama tena, ili tuweze kurejea. Ikiwa sivyo, basi tunatamani kupelekwa katika nchi nyingine”.
Wengine wameeleza matumaini yao ya kuruhusiwa kuishi kwenye nchi za ukanda.”ikiwa mpango wa kuhamishwa utaanza litakuwa ni jambo zuri,” anasema Amphile Kassim Mohamed mwenye umri wa miaka 56. “Ikiwa sivyo baadhi ya watu watataabika sana na hata kulazimika kuishi kienyeji. Uhuru wa watu kutembea unapaswa kuhamasishwa ili kuturahisishia kufanya biashara na watuj wengine.”
Vipi kuhusu jamii wenyeji?
Huku idadi ya watu katika kambi ya Dadaab ikiongezeka na kufikia karibu watu nusu milioni, haiepukiki kujikita zaidi kuwatazama wakimbizi. Hata leo hii, mtu mmoja kati ya wanne kwenye kaunti ya Garissa ambayo ina kambi – basi ni mkimbizi. Hata hivyo kaunti ya Garissa ni miongoni mwa maeneo ambayo yana maendeleo duni ya kijamii nchini Kenya, hata jamii wenyeji zinahangaika kupata huduma za msingi.
Siku moja asubuhi, Khajido Abdul Malik, alikuwa ameketi na mtoto wake wa kiume katika wodi ya watoto ya MSF kwenye kambi ya Dagahaley. Alikuwa amesafiri kwa saa tatu kwa kutumia matatu kutokea kijiji jirani cha kaunti ya Wajir. Anasema alishawahi kufika katika kilini hii hapo kabla, na kwamba hata watu wengine kutoka kwenye kijiji chake wanatumia hospitali hiyo iliyoko kambini mara kwa mara. Kanzi data ya MSF inaonesha kuwa karibu mtu mmoja kati ya watano wanapokea huduma za awali za matibabu kwenye kituo chake cha Dagahaley.
Utolewaji wa misaada ya kibinadamu kwenye makambi kunaonesha ukubwa wa tatizo na haja ya kuboreshwa kwa miundo mbinu ya msingi kwenye eneo hilo. Wakazi wengi wamekuja kutegemea zaidi huduma zinazotolewa makambini kwa miaka kadhaa, kwa hiyo kufungwa kwa kambi na kupungua kwa kiwango kikubwa kwa misaada ya kimataifa kutaathiri kwa kiwango kikubwa vijiji kadhaa.
“Ni muhimu sana kwa pande zote, wakimbizi na jamii zinazowapa hifadhi wakimbizi kuwa washirika katika kutatua mzozo wa kambi ya Dadaab,” anasema Krause. “Wakimbizi watahitaji kusindikizwa na watahitaji uungwaji mkono katika kutafuta suluhu ya kudumu. Na hili litahitaji kwenda sambamba na uongezwaji wa utoaji huduma za msingi kwa jamii wenyeji.”
MSF imekuwa ikitoa huduma za afya kwa wakimbizi wa kambi ya Dadaab katika kipindi chote cha hali tete kwenye kambi hiyo, ambapo kwa mara ya kwanza ilianza shughuli zake kwenye kambi hiyo mwaka 1991. Kwa sasa shughuli za MSF zimejikita zaidi kwenye kambi ya Dagahaley ambako inatoa huduma za msingi za afya kwa wakimbizi na jamii wenyeji ikiwemo huduma za awali na zile za juu katika vituo vyake viwili na vitanda 100 vya hospitali. Huduma zake zinahusisha elimu ya ngono na uzazi ikiwa ni pamoja na upasuji, matibabu na msaada wa kisaikolojia kwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji wa kingono na ukatili wa kijinsia, afya ya akili, sindano za kudhibiti kisukari na huduma nyinginezo. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, MSF imeshughulikia kesi 12 za dharura kaskazini mashariki mwa nchi ya Kenya ikiwemo matukio mawili ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwenye kambi za wakimbizi.
Mwaka 2018, MSF iliwahudumia wagonjwa wa nje karibu elfu 14 na wengine 860 waliolazwa kila mwezi kwenye kambi ya Dagahaley. MSF pia imesaidia kufanikisha wanawake zaidi ya 2,584 kujifungua mwaka mzima.