msf245851_medium.jpg
Access to medicines

Majanga Kujirudia

Alina mwenye umri wa miaka 3, anacheza na kaka na dada yake nyuma ya ua wa nyumba yao wakati baba yake aliposikia kilio kikubwa. Kukimbia kwenda nje, anamkuta Alina akiwa amelala chini. Hakuna aliyefahamu ni kipi hasa kilikuwa kinamsibu, lakini alikuwa kama amelala na hakuonekana kuwa mzima ; baba yake aliona wazi kuwa kuna kitu hakiko sawa kabisa. Akamnyanyua mtoto wake wa kike, akakimbilia kituo cha afya cha jirani, na wakati huo mtoto alikuwa anapata tabu kupumua. Alina aligundulika kuwa na Homa Yabisi (Pneumonia) na alianza kutumia Antibiotics ; ndani ya saa chache hali yake ikabadilika na kudhoofu zaidi ambapo alihamishiwa katika hospitali kubwa kwa kutumia pikipiki. Wakati anafika tu, Alina alikuwa tayari amekufa. Hii ilikuwa ni mwezi Februari.

Miezi michache baadae, wakati kijana wa miaka 7, Kipchoge akielekea kuchunga mbuzi wa familia, aliumwa na nyoka kwenye kidole. Mama yake haraka sana akafunga kwa kamba eneo la mguu kuzuia damu isitembee na kumpeleka mtoto wake katika kilini iliyokuwa umbali wa kilometa 5 kutoka nyumbani kwao. Katika kituo cha afya, daktari alimuhudumia kwa kumpa dawa ya kuzuia sumu na miezi michache baadae, Kipchoge aliweza kurejea nyumbani.

Watoto wote wawili walikuwa wanatoka kwenye mkoa mmoja wa Kenya, mji mdogo wa Tiaty East, kaunti ya Baringo, na wote waliumwa na nyoka wenye sumu. Lakini Kipchoge alikuwa na bahati kutokana na mzazi wake kujua kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyeumwa na nyoka, daktari aliyefahamu namna ya kugundua na kutibu tatizo, na kliniki ya jirani iliyokuwa na aina tofautitofauti ya dawa ya kuzuia sumu ya nyoka. Matokeo yake, mtoto mmoja anaishi na mwingine amekufa.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa Alina aliumwa na nyoka aina ya Black Mamba, nyoka mwenye sumu kali ambaye hushuhudiwa sana kwenye eneo lao. Sumu yake inaathiri mfumo wa fahamu na kwa haraka sana inaathiri mishipa ya upumuaji. Bila ya kupata matibabu ya haraka, hupelekea kifo. Lakini ikiwa Alina angegundulika mapema kuwa ameumwa na nyoka na kupata matibabu sahihi, pengine maisha yake yangeweza kuokolewa.

Wakati Alina alipokufa, hatari iliyokuwepo kutokana na nyoka wenye sumu lilikuwa ni suala lililoigusa kaunti ya Baringo. Hapo na maeneo mengine ya nchi, muingiliano kati ya watu na wanyama hatari unaongezeka kutokana na kuwa wote wanapigania kupata rasilimali, na matokeo yake ni kuwa idadi kubwa ya watu wamekuwa wakiumwa na nyoka wenye sumu.​

msf245857_medium.jpg

Baada ya kupata wasiwasi, wakazi wakaamua kupaza sauti, timu ya madaktari na waelimishaji jamii walitembelea eneo lao pamoja na wafanyakazi kutoka wizara ya afya kwenye kaunti na mji mdogo pamoja na washirika. Walifanya utafiti kutambua ukubwa wa tatizo, na waliwaelimisha watu kuhusu namna ya kuzuia na kutibu mtu aliyeumwa na nyoka. Na muhimu zaidi walipeleka dawa za kutosha za kuzuia sumu ya nyoka.

Upatikanaji wa dawa ya kuzuia sumu ya nyoka, sio tu dawa lakini dawa mahsusi kutibu aina ya sumu ya nyoka aliyemuuma mtu, ni tatizo sio tu kaunti ya Baringo, lakini kwenye mataifa mengi ya Afrika.

Kidunia, inaripotiwa kuwa watu milioni 2 na laki 7 huumwa na nyoka wenye sumu kali kila mwaka. Kati yao, zaidi ya watu 140,000 hufa na wengine zaidi ya 500,000 hupata ulemavu. Takwimu rasmi hata hivyo huenda idadi ikawa kubwa zaidi, wakati huu ufuatiliaji wa magonjwa kwenye nchi nyingi za Afrika na Asia ambako nyoka wengi wenye sumu hupatikana, huwa hazina rasilimali na wafanyakazi wa afya ambao hukosa ujuzi wa kubaini ikiwa mtu ameumwa na nyoka. Kifo cha Alina kisingekuwa ni kutokana na Homa Yabisi kama mtoa huduma aliyekuwepo wakati huo angekuwa na ujuzi wa kutosha kugundua.

Kwa huruma ya Alina na wengine mamia kama yeye, ni muda wa kuchukua hatua. Shirika la afya duniani limeorodhesha sumu ya nyoka kama moja ya magonjwa yaliyosahaulika, na mwezi Mei ilizindua mpango ili kuboresha udhibiti wa dawa za kuzuia sumu ya nyoka. Hatua muhimu inayofuata ni kuweka mifumo thabiti na ukusanyaji wa taarifa ili kuongeza wataalamu wenye uwezo wa kutibu mtu aliyeumwa na nyoka ; kuongeza idadi ya wafanyakazi wenye ujuzi kutambua na kutibu kidonda cha mtu aliyeumwa na nyoka ; kugawa dawa za kutosha za kutibu sumu ya nyoka ambazo zitakuwa mahsusi kwaajili ya nyoka wanaopatikana eneo husika ; na kuelimisha jamii kuhusu namna ya kupunguza hatari ya kuumwa na nyoka na namna ya kutoa huduma ya kwanza ikiwa mtu atakuwa ameumwa na nyoka.

Wakati huohuo wahanga walioumwa na nyoka, ambao huenda wakawa na matatizo ya kudumu ikiwemo kukatwa viungo, wanahitaji kutibiwa kwa kina, wakipokea tiba ya viungo na kiakili. Na ni kwa kuchukua hatua hizi ndipo tutaweza kufanikiwa kikamilifu kutibu wahanga walioumwa na nyoka kama Kipchoge na kuokoa maisha kama ya akina Alina.

* Majina yalibadilishwa.


MSF imekuwa ikifanya kazi nchini Kenya tangu mwaka 1987, awali ilifanya shughuli za matibabu nchini Sudan wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tangu mwaka 1991, Msf imekuwa ikitoa msaada kwa wakimbizi wanaowasili nchini Kenya kutokea Somalia na Sudan Kusini, huku ikitoa huduma za dharura kwa watu walio katika mazingira magumu nchini humo. MSF pia inashiriki katika kuboresha huduma za wataalamu na ubunifu kwa lengo la kusaidia jamii zilizosahaulika na changamoto nyingine za afya. Kwa mfano, MSF ilikuwa ni shirika la kwanza nchini Kenya kutoa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV) katika hospitali za uma mwaka 2001. Mwaka 2014, MSF ilitumia kwa mara ya kwanza matumizi ya dawa ya kinga ya ugonjwa Kifua Kikuu nchini Kenya ili kutibu wagonjwa wanaokabiliwa na usugu wa dawa.