Baada ya miongo kadhaa ya machafuko, mlipuko mkubwa za magonjwa ya utapia mlo, Malaria, surua na kipindupindu, inakadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 1.5 ambao hawana makazi kwenye jimbo la Borno, sasa wanakabiliwa na mlipuko wa COVID-19. Wengi wanaishi katika kambi zilizojaa msongamano huku zikiwa na uhaba wa maji na hali mbaya ya usafi, upatikanaji adimu wa mahitaji muhimu kwaajili ya usafi kama vile sabuni na maji, na mara nyingi mtu hana nafasi kabisa. Hakuna kituo cha uhakika cha afya kinachofanya kazi vizuri kwenye jimbo la Borno na uwezo wa kuwahamisha wagonjwa pia ni mdogo sana. Wakati huu watu wengi wakiwa hatarini kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko, upatikanaji endelevu wa misaada ya kibinadamu ni muhimu; Huduma ya maji na usafi lazima ziboreshwe katika makambi; na wafanyakazi walioko mstari wa mbele na wanategemewa na watu, ni lazima waweze kupatiwa vifaa kinga.
MSF imekuwa ikifanya kazi kwenye jimbo la Borno tangu mwaka 2014, na katika kipindi hiki tumeshuhudia hali ikizidi kuwa mbaya kwa wakimbizi, ambao wengi tayari wanataabika kutokana na magonjwa yaliyotokana na msongamano mkubwa, kama vile magonjwa ya mlipuko na yale ya mfumo wa upumuaji kama homa yabisi (Pneumonia), uginjwa ambao unatajwa kuwa hatari zaidi ukiambatana na COVID-19.
Operesheni endelevu za kuokoa maisha
Ugonjwa wa COVID-19 tayari umekuwa na athari kubwa katika mifumo ya afya, uchumi wa nchi na watu duniani na unaashiria hatari kubwa kwenye jimbo la Borno. Hata hivyo, hata kama COVID-19 isingekuwepo nchini Nigeria, uhitaji wa misaada ya kibinadamu kwenye mji wa Borno bado ungekuwa mkubwa. Katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja, msimu wa mvua utaanza, ikija sambamba na kesi za wagonjwa wa malaria na utapia mlo. Maiduguri, Ngala, Pulka na Gwoza, hospitali zetu zinafanya kazi saa 24, siku saba za wiki, na wakati wa msimu wa mvua zitajaa. Mwaka 2019 peke yake, MSF iliwatibu wagonjwa zaidi ya 10,000 kutokana na utapia mlo jimboni Borno na zaidi ya wagonjwa 33,000 wa malaria; na wengine zaidi ya 40,000 walihudumiwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi.
Athari ambazo ugonjwa wa COVID-19 utasababisha kwa wagonjwa wetu hazipaswi kupuuzwa, lakini ikiwa athari itakayosababishwa na ugonjwa huu itaruhusiwa, utolewaji wa misaada ya kibinadamu, matokeo yake yatakuwa ni ya kutisha sana.
MSF inaguswa sana na kuenea kwa maambukizi ya COVID-19 na uwezekano wa athari utakaokuwa nao kwa watu walio kwenye mazingira magumu. Wakati huu virusi hivi vikienea Nigeria, kipaumbele chetu ni kuhakikisha operesheni zetu zinakuwa endelevu kuokoa maisha ya maelfu ya watu kila mwaka, na kuwalinda wagonjwa na wafanyakazi wetu. Kufanya haya, matabibu wetu na timu za ugavi wameweka itifaki wa kuzuia, kuzitaarifu jamii kuhusu njia rahisi zaidi za kujikinga dhidi ya COVID-19, kutenga maeneo ya kunawa mikono kwenye jamii, kutengeneza maeneo ya kuwatenga watu na kuakisi taratibu zetu za kimatibabu. Wakati huu wa mahitaji makubwa ya upatikanaji wa dawa, manunuzi ya vifaa kinga kwa wafanyakazi wa afya imekuwa changamoto, hata hivyo ni changamoto ambayo ni lazima tuikabili kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wa afya walioko mstari wa mbele na kuendelea kuwatibu wagonjwa wetu.
Maji safi na salama: Kitu cha thamani na uhaba wa rasilimali
Pulka, ambako MSF ina hospitali na inatoa elimu kwa uma, upasuaji, huduma za uzazi na matibabu kwa wahanga wa ubakaji na ukatili wa majumbani, hali ni mbaya. Pulka ni mji uliotengwa; eneo ambalo liko chini ya udhibiti wa jeshi la Nigeria. Hivi sasa ni eneo la makazi ya watu 63,000, asilimia 78 kati yao angalau walishakimbia nyumba zao mara moja tangu mwaka 2015. Kuna jumla ya watu 27,000 wanaoishi katika kambi zilizojaa kwenye mji wa Pulka huku kukiwa na uhaba wa huduma muhimu, ikiwemo maji, chakula na huduma za afya. Kote kwenye miji wa Pulka na Gwoza (miji inayopakana), kambi za muda wa wahamiaji wapya sasa zimejaa; Kwenye eneo la Gwoza, idadi ya watuj ni mara tatu zaidi ya ile inayopendekezwa; na Pulka, mahema yanatoa hifadhi kwa watu kwa zaidi ya miezi au hata miaka wakati yalitengenezwa kuwa makazi ya muda kwa angalau majuma kadhaa wakati suluhu ikitafutwa.
Katika tathmini ya hivi karibuni kuhusu maji na hali ya usafi, MSF ilibaini kuwa ugavi wa maji kwa mtu mmoja kwenye kambi ya Pulka ilikuwa ni lita 11, ikiwa ni kiwango cha chini sana tofauti na miongozo ya misaada ya kibinadamu ambapo inahitajika angalau lita 20 kwaajili ya afya na usafi. Na katika lita hizi 11 ni wastani wa lita mbili tu ambazo zilizekewa dawa ya Chloride na salama kwa kunywa. Pia ilirekodi upatikanaji wa lita 4.5 kwa mtu katika tathmini zilizopita:
Unatakiwa kuamka mapema ikiwa unataka kupata maji ya kutosha…..nina watoto saba, na wakati mwingine majik hata hayatoshi kwa sisi kunywa – wakati mwingine inabidi kuwabembeleza majirani zetu watupe maji ya kunywa. Kila siku wanawake visimani wanagombana kisa maji – tunajua hayatakaa yatoshe kwa kila mtu.
- Ajia Adam,
Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno, upatikanaji wa maji na hali ya usafi sio ya kuridhisha pia. Kati ya mwaka 1999 na 2011, MSF ilienda zaidi ya mara saba kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu kwenye mji wa Maiduguri, na mwaka 2018, watu 4,000 waligundulika kuwa na kipindupindu katika maeneo 18 ya Borno, Adamawa na jimbo la Yobe.
“Katika kambi zote ambazo MSF inafanya kazi kwenye jimbo la Borno, ombwe katika upatikanaji wa maji na maeneo ya usafi yanatishia zaidi mlipuko wa COVID-19. Ombwe hili linachangiwa na idadi kubwa ya watu, masuala mtambuka ya afya na kushindikana kushughulikia miundombinu, yanaonesha wazi hatari iliyoko kwa raia. Hakuna shaka yoyote kuhusu hatari itakayoletwa na mlipuko wa COVID-19, hata hivyo, jambo moja tunalolifahamu kwa hakika, magonjwa mengine na hali nyingine za kiafya hazitasaza watu. Kamwe hatuwezi kukubali kuona mlipuko huu unaathiri misaada ya matibabu – utolewaji wa huduma za matibabu kwa wakati huu ni muhimu sana na itaokoa maisha.” anasema Siham Hajaj, mkuu wa tume ya MSF.
COVID-19 sio tishio pekee linalowakabili watu wa jimbo la Borno, lakini uwepo wake tu nchini Nigeria kunatoa ishara ya hali tete inayowakibili raia wengi ambao tayari wamesumbuliwa na hali ya vita, magonjwa na utapia mlo. Kwao wao, suala la kuachiana nafasi ni msamiati, na uoashaji mikono wa mara kwa mara unadumaza rasilimali hii. Katika mazingira ya mlipuko huu, kuharibika kwa mifumo ya afya kwenye jimbo la Borno ni suala ambalo liko wazi kabisa. Ni jambo la muhimu sana kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu unakuwa endelevu kwa watu hawa. Kushindwa kufanya hivyo kutagharimu maisha.