Zaidi ya watu 45,000 wamethibitishwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kaunti ya Turkana, huu ukiwa ni moja kati ya milipuko mibaya zaidi kushuhudiwa kwenye kaunti hiyo tangu mwaka 2017. Mwishoni mwa mwezi Septemba, Msf ilituma timu yake ya dharura kusaidia kaunti hiyo kukabiliana na mlipuko wa Malaria baada ya kufanya tathmini ya mahitaji na ombwe lililokuwepo katika kudhibiti maambukizi.
Timu ya wataalamu hawa imekuwa ikiendesha kampeni ya uelewa, kwa kwenda katika maeneo yaliyoathirika kwa kuwapima na kuwatibu watu waliobainika kuwa na malaria na maradhi mengine. MSF iliwaona wagonjwa 2,742 katika wiki ya kwanza tangu iwasili, kati yao hao watu 969 walithibitishwa kuwa na malaria na walianza mara moja matibu.
Kaunti ya Turkana Magharibi tu imerekodi kuwa na idadi kubwa ya kesi za malaria ambapo ni zaidi ya asilimia 65 ya wagonjwa waliopimwa kuthibitishwa. Timu ya MSF ilitembelea maeneo ya Loririt, Nawatom, Loita, Nalapatiu, Narukirionok na Nasinyono kaunti ya Turkana Magharibi. MSF pia ilitoa huduma ya matibabu kwenye maeneo ya Lokalolio, Nakiria, Moruongor, Lokorimoru, Namerisinyen, kata ya Township na maeneo mengine ya Turkana Kati. Juhudi za MSF zilijikita katika kaunto hizi mbili ambazo ndizo zimeathirika pakubwa kwa sasa.
Moja ya kikwazo kwa sasa ni mvua kubwa iliyonyesha kwenye maeneo haya, ambapo imefanya kuwa vigumu kufikia baadhi ya maeneo ili kutoa huduma za matibabu, huku baadhi ya familia zikiamua kuwaweka nyumbani wagonjwa kutokana na hali mbaya ya hewa.