Beledweyne ni mji mkubwa ulioko katikati mwa nchi ya Somalia, ukiwa na majengo marefu na ni mji wa kibiashara. Licha ya kuwa kimsimu huathirika na mvua, mwaka huu ilikuwa tofauti. Mto Shabelle ulifurika maji kutoka katika milima ya nchi jirani ya Ethiopia, ambapo mwezi October kingo zake zilipasuka na kwa kiwango kikubwa kufurika mjini.
Mafuriko yamemuathiri kila mtu, tajiri na masikini, kwa kiwango ambacho hata wazwa hawajawahi kukiona. Kila mtu alilazimika kutoka nyumbani kwake na kwenye maofisi. Baadhi ya watu walilazimika kupanda juu ya bati na kutengwa; wengine waliokolewa na boti kutoka kwenye nyumba zao.
Eneo la mlipuko wa magonjwa
Baada ya siku chache za bila ya mvua, maji sasa yameanza kupungua, lakini madhara kwenye barabara na mifereji yanaonekana wazi. Mifereji ya maji na mafuriko yamechanganyika, na kwa kiasi kikubwa yamechafua visima ambavyo vinatoa maji safi ya kunywa. Hifadhi za chakula zimesombwa na maji na masalia ya vidimbwi vya maji vinaonekana kila mahali, hali inayofanya kuwa sehemu ya mazalia ya mbu wanaosababisha malaria na magonjwa mengine.
Hospitali ya wilaya ilifunikwa na maji karibu nusu mita. Ni chumba cha upasuaji pekee ambacho kiko mbali kidogo na maeneo mengine hakikuathirika na maji. Huduma za kuonana na madaktari zilisimama na hospitali imeshindwa kufanya kazi katika kipindi cha majuma matatu. Mfumo wa umeme unawezekano mkubwa kuwa uliharibiwa na tena dawa na vifaa vingine vya matibabu huenda visitumike tena.
Idadi kubwa ya watu kukosa makazi.
Katika kipindi kifupi, mafuriko yalisababisha watu karibu laki 270,000 kwenye mji wa Beledweyne kukosa makazi, hii ni kwa mujibu wa ofisi ya umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu. Walienda kwenye maeneo ya juu ya magharibi na mashariki mwa mji. Wengi hivi sasa wanaishi katika mahema ya muda, ambayo mengi yametengenezwa kwa nguo au miti. Itachukua muda kidogo mpaka waweze kurejea kwenye nyumba zao.
Tuliwasili tukiwa na timu ya watu wachache kwenye mji wa Beledweyne, Octoba 31. Katika kile kilichotarajiwa kuwa kufanya tathmini ya kawaida kiligeuka na kuwa hali ya dharura kutoka na uhitaji uliokuwepo. Licha ya kufungwa kwa uwanja wa ndege kwa siku kadhaa, tuliweza kusambaza vyakula; mahema; na vifaa vingine ambavyo si chakula kama vile mablanketi, ndoo na mafuta ya kupikia kwa kutumia barabara. Pia tulijenga vyoo na kusafirisha maji safi na salama.
Watu wengi wanaishi katika hali ya hatari jambo ambalo mara zote imekuwa ni vigumu kuamua nani ana uhitaji wa haraka. Nimeshuhudia watu wazima na watoto wakilazimika kuishi pamoja kwenye mahema na makazi ya muda ya nguo na miti kwa sababu hapakuwa na malazi ya kutosha familia nzima. Nimeshuhudia wanawake wakijifungua katika mazingira machafu na mwanamke aliyekuwa na utapia mlo akihangaika baada ya kumpoteza mume wake na hawezi kunyonyesha watoto wake mapacha kutokana na njaa.
Mpaka sasa msaada uliogawanywa umekuwa kama tone la maji baharini
Siku moja wakati tukifanya tathmini ya eneo moja lililoathirika, niliguswa kumuona mama mmoja ajuza akiomba hifadhi katika moja ya malazi ya muda. Siku chache baadae tuliporudi kutoa hema, ilikuwa tumechelewa sana. Tuliambiwa alishafariki.
Mpaka sasa msaada uliogawanywa umekuwa kama tone la maji baharini. Baadhi ya familia zinagawanya chakula cha kuongeza nguvu kijulikanacho kama Plumpy’Nut, ambacho hutolewa kwa watoto kwaajili ya tiba ya utapia mlo. Baadhi wameamua hata kunywa maji ya mvua. Wengi hawana cha kujikinga wakati wa jua kali, joto na baradi nyakati za usiku.
Timu ya pili ya MSF iliwasili wiki moja baadae. Baada ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa wizara ya afya, walianzisha kliniki zinazotembea katika maeneo manne tofauti ya mjini.
Tunaona mateso mengi. Watoto wanaletwa wakiwa na matatizo ya mfumo wa hewa kama vile baridi yabisi (pneumonia). Tunatibu magonjwa mengi ya mlipuko, hasa Malaria, kuharisha na homa ambazo vyanzo vyake havijulikani.
Maradhi ya utapia mlo tayari yalikuwa ya kiwango cha juu hata kabla ya matatizo, lakini sasa hali imezidi kuwa mbaya na watoto wenye hali mbaya ya utapia mlo wamekuwa wakiwasili kwaajili ya kuonana na madaktari.
Tuna wasiwasi kutokana na uwezekano wa kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine ya mlipuko kama kipindupindu. Juhudi za haraka na uratibu wa pamoja miongoni mwa mashirika ya misaada ya kibinadamu pamoja na mamlaka za nchi zinahitajika ili kuendelea kuhamasisha misaada na kuhakikisha misaada inawafikia watu wanaohitaji katika muda muafaka.
Ni muhimu sana kwa sasa kuboresha uoatikanaji duni wa maji na mazingura safi kwenye mji wa Beledweyne na kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa ili kuepuka kuenea kwa magonjwa.